Headlines:

         

EXECUTIVE BRIEFING TO THE PRESIDENT OF THE REPUBLIC OF BURUNDI H.E. PIERRE NKURUZINZA VISIT TO THE PORT OF DAR ES SALAAM  27TH NOVEMBER, 2006
Deputy Minister for Infrastructure Hon. Maua Daftari speech to H.E Azali Assoumani President of Union of Comoros
TPA Chief Executive Mr. Mtandu Presentation to H.E Azali Assoumani President of the Union of the Comoros
Concessioning or privatization as a better option for African ports: Case of Dar es Salaam port by Samson Luhigo - TPA CEO
Presentation by TPA CEO, Mr. Samson Luhigo: Challenges of African Ports at IAPH Africa-Europe Meeting London March 9-11
SPEECH BY TANZANIA HARBOURS AUTHORITY CHIEF EXECUTIVE OFFICER, MR. SAMSON LUHIGO ON THE OCCASION OF THE OPENING CEREMONY OF THE 3RD INTERMODAL AFRICA CONFERENCE, DAR ES SALAAM FEBRUARY3RD, 2005
Rasimu ya hotuba ya Naibu Waziri wa mawasiliano na Uchukuzi
HOTUBA FUPI YA MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA
HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI WA MAMLAKA YA BANDARI
Tanzanian port has big aspirations:Tanzania's success story

 

 

RASIMU YA HOTUBA YA NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA UCHUKUZI, MHESHIMIWA DR. MAUA A. DAFTARI – MBUNGE – YA KUZINDUA BARAZA JIPYA LA WAFANYAKAZI LA MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA, APRILI 12 2003, DAR ES SALAAM

Ndugu Mwenyekiti wa Bodi
Ndugu Mwenyekiti wa Baraza
Ndugu Katibu wa Baraza
Ndugu Wajumbe wa Baraza

Ndugu Mwenyekiti,

Nashukuru sana Ndugu Mwenyekiti na Baraza lako kwa kunialika kuja kuzindua Baraza hili jipya mlilolikamilisha kwenye uchaguzi wenu hivi karibuni.

Nimetaarifiwa katika mwaliko kwamba hii ni awamu ya nane ya Baraza la Wafanyakazi kwa Mamlaka.

Mabaraza ya Wafanyakazi na hasa hili la Bandari, yana umuhimu wa kihistoria. Historia hiyo kwenye taasisi nyingi imekuwa ni ya mafanikio. Baraza la bandari ni chombo chenye nafasi pekee katika
uchumi wa kanda kubwa ya Afrika ya Mashariki na Kusini, hivyo ipo haja mnapokaa kupanga mambo yenu, muwe na mipango thabiti mnayoweka ambayo itakuwa ni mikakati muhimu ya malengo ya taasisi za biashara nchini na kwa majirani kwa ujumla.

Ndugu Mwenyekiti,

Umuhimu wa ushirikishwaji wa wafanyakazi unaeleweka, ingawaje ushirikishwaji wenyewe hubadilika kila mara mazingira ya uchumi, mifumo ya uendeshaji wa taasisi, na sasa hata utandawazi unavyoongezeka. Hivyo ushiriki wenu na menejimenti ya shirika lazima uendane na wakati na usiwe ule wa miaka iliyopita.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza,

Dunia ni biashara, na kwa dunia ya sasa ya utandawazi, mazingira yamepelekea kupanuka na kuongezeka sana shughuli za uchumi na biashara. Utandawazi unasababisha bidhaa zisafirishwe nchi hadi nchi kwa wingi na kwa kasi zaidi. Ili hili liwezekane, tunahitaji kuwa
na mfumo imara wa mawasiliano na usafirishaji na pia kuondokana na urasimu katika shughuli zenu.

Wafanyabiashara wengi, na hasa wale wa mahitaji ya kila siku wananunua toka popote pale duniani ambapo wanaonelea kwamba bei ni nafuu kwao na huduma zao wanazipata kwa urahisi zaidi.

Ili kukabili changamoto za maendeleo haya, bandari zitaendelea kuwa sehemu muhimu na nyeti kwenye mtandao wa usafirishaji ulimwenguni.

Bandari hivi sasa zinatakiwa kushindana katika ubora wa huduma na wala si wingi wa shehena tena. Ukitoa huduma bora, basi utajiuza bila jasho na shehena zitajileta zenyewe.

Ndugu Mwenyekiti,

Changamoto la mipango ya Baraza hili ni kupambana na kasi ya maendeleo ya mifumo ya uchumi, na kuwahakikishia watumiaji wake huduma bora saa na siku zote.

Mabadiliko ya mazingira ya uchumi yanatupa changamoto ya kubadilisha mifumo ya vyombo vyetu. Changamoto hii ndiyo iliyoleta pambazuko la ubinafsishaji. Lakini leo hatutazungumzia chimbuko au
mantiki yake. Nyie kama wajumbe mmekwisha pata semina nyingi tu juu ya ubinafsishaji na mnafahamu vyema suala zima, Hivyo tukubaliane tu kwamba, Mamlaka ina uzoefu na utaalamu wa kutosha katika ubinafsishaji na mmepata nafasi ya kushirikishwa katika zoezi hili zima.

Ubinafsishaji, ndiyo dawa pekee ambayo ingeleta ubora na kiwango kikubwa cha ufanisi na tija, bila kusahau kuongezeka kwa mtaji.

Ndugu Mwenyekiti,

Hatua za kubinafsisha shughuli za sekta ya usafirishaji wa baharini na nchi kavu sasa zinafikia kikomo. Maandalizi yote yamekamilika na kilichosalia ni utekelezaji. Maandalizi ya ubinafsishaji katika sekta nyingine za usafirishaji nazo zinaenda vyema kulingana na mipango yetu; mathalani Shirika la Ndege la Tanzania tayari limekwisha binafsishwa na ubora wa huduma zake sasa unaonekana wazi.

Pia, Kituo cha Kontena ndicho kitengo cha kwanza katika Mamlaka kubinafsishwa, na sasa kinatumika kama kigezo cha mafanikio. Idadi ya makontena imeongezeka, masoko yanaimarishwa na kero zilizokuwa zinatokana na urasimu wa mashirika ya umma zimeondolewa.

Kwa mujibu wa ratiba ya ubinafsishaji wa vitengo vilivyosalia kwenye Mamlaka unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2004 ambapo waendeshaji binafsi wanatarajiwa kupatikana. Wakati huo Serikali itabadilisha muundo wenu. Mamlaka mpya inatarajiwa kuanza kazi Januari 2005. Mamlaka mpya inatarajiwa kupewa jukumu la kudumisha huduma za kibandari, dhamana ya kusimamia rasilimali za bandari na kuhakikisha kuwa mikataba mbali mbali iliyowekwa ya uendeshaji wa shughuli za bandari inafuatwa.

Ndugu Mwenyekiti,
Utaratibu na mwenendo wa ubinafsishaji wa shughuli zilizobakia umeipa Mamlaka na nyinyi wenyewe fursa mpya iliyokosekana pale tuliposhughulikia masuala ya ubinafsishaji awamu ya kwanza.

Naamini nafasi itakuwepo kwa Watanzania, na wafanyakazi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika shughuli za uendeshaji wa vitengo
vilivyobakia. Naomba nafasi hiyo ikijitokeza muitumie kikamilifu kwa kufuata taratibu zitakazowekwa.

Naelewa yapo maswali mawili ya msingi ambayo mgependa kujua hatima yake. Nayo ni mafao yenu na nyumba. Napenda niwahakikishie masuala hayo yatafanyiwa kazi ipasavyo. Sina shaka hatima njema itapatikana kwa maslahi ya wote.

Ndugu Mwenyekiti na ndugu wanabaraza,

Napenda nimalize hotuba yangu kwa kutoa nasaha chache kwenu nazo ni:

Kwanza, umuhimu wa kuhifadhi maisha yenu kwa kujikinga na balaa kubwa la gonjwa wa Ukimwi. Janga hili limepoteza wengi wenu na litaendelea kupoteza wengine na kuacha athari mbaya kiuchumi kwa familia na nchi kwa ujumla.

Ni muhimu sana wakati huu mkaweka mpango kabambe na kuusimamia kwa uwezo wenu wote kwa kuendelea kujielimisha na kujikinga dhidi ya ugonjwa huu na kuhifadhi maisha yenu.

Pili, mtakumbuka Mamlaka iliwapatia nafasi ya kuwafunza namna bora ya kujiendeleza mtakapostaafu ili muweze kuishi maisha endelevu, kwa kujizatiti na kubuni mbinu mbali mbali za kujipatia vipato. Hivyo kumbukeni kuyatumia ipasavyo mafunzo hayo.

Tatu, ufanisi mkubwa bandarini, huleta sifa nzuri na kuwavutia washitiri kutumia bandari zetu. Aidha ufanisi mzuri unategemea
kuwepo kwa vifaa vya kisasa na wafanyakazi wanaojituma kwa ari yao wenyewe.

Biashara ya nchi jirani, inaweza kabisa kuwa ni biashara ya nchi yetu. Kwa nchi yetu, biashara hii ni mgodi ulioko nje ya nchi. Inafahamika kwamba mathalani Uganda inasafirisha tani milioni moja za bidhaa zake kwenda au kutoka nchi za mbali. Katika shehena hiyo, takwimu zenu zinaonyesha kuwa bandari zinaambulia asilimia kumi na tano tu. Kiwango kama hicho pia kinalingana na kile kitokacho Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Tujiulize hapa kwa nini karibu shehena yote toka Uganda ipitie bandari za nchi nyingine badala ya Dar es Salaam au Tanga ama Mtwara.

Hivyo, juhudi zenu na Serikali sasa hazina budi kuelekezwa kuivutia shehena hiyo kwa mikakati mbali mbali kama kujitangaza zaidi, kurahisishwa taratibu za uingizaji na uondoshaji mizigo bandarini, usalama wa mizigo bandarini, kushirikiana zaidi na vyombo vya usafirishaji, pamoja na kuimarisha mawasiliano kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Lakini nyie kama wafanyakazi mnapaswa kuchangia zaidi kwa kuwa na mwamko wa kibiashara ya ushindani, kinyume na ukiritimba.

Mwenyekiti,
Hatimaye basi niwatakieni heri katika majukumu yenu na hasa hili la uwakilishi katika chombo hiki muhimu katika Mamlaka. Huenda huu ni wakati mgumu na tofauti kuliko historia yenu ya Baraza, lakini hapana shaka safari ndefu ya mafanikio itawatulizeni kituoni salama
salimini. Baada ya kusema hayo napenda nitamke rasmi kuwa baraza lenu limezinduliwa rasmi.


HOTUBA FUPI YA MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA BWANA SAIDI KASSIM WAKATI WA UZINDUZI WA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI APRILI 12, 2003 DAR ES SALAAM

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,
Dr. Maua Abeid Daftari
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Bwana Samson Luhigo
Ndugu Katibu, Henry Kivo
Ndugu Wajumbe,
Waandishi wa Habari na Wageni, Mabibi na Mabwana

Mheshimiwa Naibu Waziri

Kama alivyoanza Mwenyekiti wa Baraza, nami hali kadhalika napenda nikupe shukurani kwa niaba yangu mwenyewe binafsi, na kwa niaba ya Baraza la Wakurugenzi, na ama hakika wafanyakazi wote katika Mamlaka wanoawakilishwa na wajumbe waliopo hapa asubuhi ya leo.

Wanasiasa wanakuwa na kazi na shughuli kila siku ya maisha yao, hata wawapo likizoni, na mwanasiasa huyo anapopewa wadhifa mwingine kama wa uwaziri, basi kama alivyosema mwenyewe Mheshimiwa Rais, anakuwa ametwishwa uaskari, na hapa kwetu anatakiwa awe kama askari wa mwamvuli.

Ninafurahi kwamba unaumudu uaskari wako, kwani shughuli ya leo hapa, ni mojawapo tu kati ya mlolongo wa majukumu makubwa yanayokukabili. Kama alivyotamka Mwenyekiti wa Baraza, juma hili linawamalizia ngwe mliyokuwa nayo huko Bungeni Dodoma.


Mimi binafsi, nimefurahi kwamba umeweza kuwepo hapa, kwani, kazi yote inayofanyika katika Baraza hili, hatima yake ni mapendekezo yanayoletwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi. Na Bodi nayo, itakapomaliza kazi ya kuzichambua hoja zitakazotoka hapa, inapendekeza kwa Wizara yetu ya Mawasiliano na Uchukuzi ambayo unaiongoza wewe.

Tunafarijika sana kwamba kwa vipindi vyote, vyombo vyote vya Mamlaka, yaani Baraza hili, na Bodi yangu, vimeweza kupendekeza mipango ambayo yalipofika mbele yako, imepokelewa na kuidhinishwa.

Sisi katika Bodi tunalitazama Baraza hili kama chombo cha ufanisi, kwani limetuwezesha kufanya kazi na dhamana tuliyokabidhiwa ya chombo hiki kwa ufanisi na imani ilivyotarajiwa. Ningependa kuchukua fursa hii kumpongeza mwenyekiti wao na wajumbe kwa ujumla na papo hapo kuwasihi wasije wakabweteka, na kulegeza kamba, hata hapo muundo wa Mamlaka utakapokuwa umebadilika kabisa.

Ama kwa hakika nitoe tahadhari hapa kwamba pamoja na kwamba wamesema wamekuwa wakifanya kazi zao kuiushindani ndani ya mfumo wa ukiritimba, ushindani katika soko huria ni mkubwa na mgumu zaidi.

Baraza halina budi kujipima na kuhakikisha kwmba linaziba mapendgo yoyote yale miongoni mwao yatakayobainika kuwa ni udhaifu hapo wanapoingia kwenye vita vya biashara huria.

Mheshimiwa Naibu Waziri

Kazi yangu hapa ni kukukaribisha kwenye hadhara, hivyo nisiseme mengi bali tu nikuahidi kwamba tayari tupo kwenye kipindi cha kuandaa mipango ya mamlaka kwa kipindi kijacho, na juma lijalo tutakuwa tumeikamilisha na kuiwasilisha kwenu kwa wakati unaotakiwa kisheria.

Mheshimiwa

Karibu hadhara hii ya wajumbe ni yako wewe sasa.

HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI WA MAMLAKA YA BANDARI BWANA SAMSON M.E. LUHIGO WAKATI WA UZINDUZI WA BARAZA APRILI 12, 2003 DAR ES SALAAM

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,
Dr. Maua Abeid Daftari
Mwenyekiti wa Bodi Bwana Saidi Kassim
Ndugu Katibu, Henry Kivo
Ndugu Wajumbe,
Waandishi wa Habari na Wageni, Mabibi na Mabwana

Mheshimiwa Naibu Waziri,
Kwa niaba ya Baraza hili, ninapenda kuelezea furaha na shukrani zetu kwako wewe binafsi, Serikali na hasa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kutupa fursa na heshima na muda wako kuzungumza na moja ya vyombo muhimu sana kwenye Mamalaka ya Bandari Tanzania, yaani Baraza la Wafanyakazi.

Tunafahamu kuwa majukumu mliyonayo kwenye ofisi zenu wenyewe ni mazito na makubwa lakini pamoja na yote hayo, imepatikana nafasi ya kuja hapa na kutupa mwangaza wa kutazama wajibu tulio nao kama Mamlaka.

Nikisema uzito wa kazi zenu, ninazingatia kwamba kwa majuma mawili sasa Bunge limekuwa likikutana na Wizara yako hasa, na imekuwa na muswada mzito wa uanzishaji wa Mamlaka ya Uthibiti wa Mawasiliano (Communications Regulatory Authority).

Mheshimiwa Naibu Waziri,
Kisha kutoa shukurani kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya wajumbe wa Baraza, napenda kuelekeza mtazamo wangu kwenye dhima ya Baraza la Wafanyakazi, na Mamlaka ya Bandari.

Hii ni awamu ya nane ya miaka mitatu mitatu ya Baraza hili. Mamlaka imekuwa mbele katika utekelezaji wa agizo la Serikali la miaka thelathini na zaidi ya ushirikishwaji wa wafanyakazi kwenye kuweka wenyewe mipango ya uchumi ya shirika walilodhaminiwa kuliendesha, tangu lilipoanzishwa, mwaka 1977.

Hili ni Baraza Kuu. Linakuwa Kuu kutokana na kuwepo katika Mamlaka vituo vikuu vitatu vya kazi ambavyo ni Makao Makuu, na Bandari tatu za Dar Es Salaam, Tanga na Mtwara. Muundo katika kila baraza la kituo ni wa vikundi vitatu vya wafanyakazi. Kwanza ni Menejimenti ambao huingi a katika baraza kwa mujibu wa ofisi zao, na pili ni chama cha wafanyakazi ambao huwakilishwa na viongozi wake akiwemo mwenyekiti na katibu wake. Kundi la tatu ni wawakilishi wa wafanyakazi ambao huchaguliwa na wafanyaakazi kutokana na idara zao.

Baraza Kuu linaundwa na Menejimenti kutoka kituo cha Makao Makuu, Vuingozi wa vituo vyetu vitatu, viongozi wa vyama vya wafanyakazi katika vituo vyote, na wawikilishi wa wafnayakazi waliochaguliwa toka kwenye mabara ya vituo.

Vyombo vya kazi katika mabaraza yote ni Kamati za utendaji na Baraza Kuu lenyewe. Kamati ya Utendaji inafanya kazi kubwa ya kupitia mapendekezo ya vituo kisha kuyawasilisha kwenye baraza kuu.

Mwaka huu, tumekuwa na upungufu kidogo katika kuanza kwa shughuli za Baraza . Kutokana na mtazamo mpya wa wafanyakazi, wameamua kuunda chama kipya kinachojumuisha wafanyakazi wa bandarini pekee, yaani dockworkers, na kujitoa katika fungamano la awali la vyombo vya mawasiliano.

Taratibu zao za kujiandikisha zimewachukua muda na hadi. Uwakilishi wao katika kipindi hiki, kwa vituo ambavyo tayari vilikuwa vimejitoa kisheria na chama chao, haukuwezekana isipokuwa kwa bandari ya Dar Es Salaam.

Hata hivyo tunatarajia kwamba tutawapata washiriki hao katika vikao vijavyo vya baraza.

Kazi ya Baraza katika vikao vyake vinavyofanyika mara mbili kila mwaka wa fedha ni kujadili malengo, faida na matumizi ya kutokana na matarajio ya shehena na pato letu. Mamlaka ina malengo thabiti manne makuu ya kazi zetu, ambayo ni; mosi kuendelea na utekelezaji wa zoezi la ubinafsishaji, pili kutoa huduma kwa ufanisi kwa wateja wetu kila wakati, tatu kupata ziada ya kutosha kulingana na rasilimali iliyopo, na nne kulinda idadi sahini ya wafanyakazi wenye ujuzi kikamilifu na ari.

Katika malengo haya yapo matatizo mengi, lakini mimi ningependa kuyaita ni ‘challenges’. Baraza hili linayapitia matatizo haya na mikakati iliyotayarishwa ya kuyakimu, na ningependa nitaje tu hapa kwamba nyakati zote limeweza kuishauri menejimenti na bodi kwa ufanisi mkubwa.

Baraza limekuwa likiendesha shughuli zake kwa mihula yote hiyo kwenye mfumo wa ukiritimba na kama taasisi ya Umma. Pamoja na ukiritimba, naweza kukiri kwamba wakati wote tumekuwa na mtazamo halisi wa ushindani na kuwa na mafanikio makubwa.

Lakini mtazamo wa biashara na uchumi hivi sasa umebadilika na baraza halina budi kufuata dira hiyo hiyo.

Mfumo wa Mamlaka hivi sasa unafanyiwa marekebisho sambamba na uhuishwaji wa shughuli za uchumi na sekta binafsi. Kwa mwendo huo hapana shaka huu ni muongo wa mwisho wa mfumo huu wa Baraza kwa Mamlaka ya Bandari. Mabaraza yafuatayo, japo yatakuwa bado ni ya uchumi, yatakuwa na malengo tofauti na sasa.

Tayari sehemu muhimu zaidi kiuchumi na utendaji kazi – Kitengo cha Makontena kimekwisha pangishwa yapata miaka mitatu na zaidi.

Hali ya utendaji katika kitengo hicho kama tunavyoifuatilia ni ya kuridhisha, na mwendeshaji huyo – Tanzania International Container Terminal Services Ltd., (TICTS) ameweza kuendeleza na kuboresha misingi mizuri ya kazi na vitendea kazi alivyorithi toka Mamlaka.

Kazi ya ubinafsishaji iliyobakia ni ile ihusuyo kitengo cha shehena za kawaida na zile huduma nyingine za kibiashara kwenye bandari ya Dar es Salaam pamoja na bandari za Tanga na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Waziri,
Katika hatua zitakazofuata za ubinafsishaji vitengo vilivyosalia, Mamlaka imelenga vyema na inawaandaa wafanyakazi kupata fursa ya kushiriki kama wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Waziri,
Naomba nishukuru tena na nimuombe Mwenyekiti wetu wa Bodi, Mzee Saidi Kassim achukue fursa yake rasmi kukukaribisha uweze kuzungumza na wajumbe.

Top